top of page

Simon Group Yadhamini Pambanola Azam Na Yanga


KAMPUNI ya Simon Group ya mjini Dar es Salaam , imejitosa kudhamini pambano la hisani kuchangia walemavu kati ya Mabingwa watetezi Yanga na Azam FC.

Pambano hilo linalosubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki wa timu zote, litarajiwa kufanyika keshokutwa katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam .

Tayari timu zote zimeanza tambo na ziko kwenye mazoezi makali kila mmoja ikijipanga kutoka na ushindi na kutumia mchezo huo kujiandaa na mzunguko wa pili wa ligi kuu.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Dar es Salaam , jana, Mratibu wa Asasi ya Unity in Diversity Foundation (UDF) Enock Bigaye, alisema Somon Group ni mmoja wa wadhamini wakubwa wa mchezo huo.

Alisema Mkurugenzi wa Simon Group, Robert Kisena, amekuwa karibu katika kufanikisha mambo mbalimbali ya asasi hiyo na kwamba, ameguswa na kusaidia jamii ya walemavu.

“Simon Group imekuwa mdau mkubwa wa UDF, inatusaidia katika mambo mbalimbali na imewezesha maandalizi ya mchezo huo kwa kubeba baadhi ya gharama. Tunaishukuru sana na tunaomba wengine waige mfano huu,” alisema Bigaye.

Alisema mbali na Simon Group, wadau wengine wa UDF ambao wamekuwa wakisaidia katika masuala mbalimbali ni Katibu wa NEC ya CCM, Itikadi na Uenezi, Mwigulu Nchemba.

Wengine ni Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philip Mulugo, ambaye anatarajiwa kuongoza ujumbe wa wabunge zaidi ya 10 kushuhudia pambano hilo baina ya Yanga na Azam FC.

Pia, wamo Vick Kamata (Viti Maalumu-CCM), Munde Tambwe (Viti Maalum-CCM), Abdalah Kigoda (Handeni), ambao wanatarajiwa kushuhudia mpambano huo.

Akizungumzia kuhusu pambano hilo la keshokutwa, Bigaye alisema maandalizi yote muhimu yamekamika na kwamba, Mkuu wa Mkoa Dar es Salaam , Said Meck Sadiq atakuwa mgeni rasmi.

Alisema timu zote ziko kwenye maandalizi makali kwa ajili ya mchezo huo. Yanga jana ilikuwa dimbani kuchuana na JKT Ruvu, katika mchezo wa kirafiki.

bottom of page