top of page

December 19, 2011

MECHI YA HISANI YANGA VS. AZAM KESHO

JUMANNE iliyopita, Desemba 13, 2011, dunia ya wapenda soka ilikuwa ikishuhudia pambano la hisani lililo katika mradi, ‘project’ maalumu iliyopewa jina la ‘Match Against Poverty’ iliyopigwa ndani ya dimba la Hamburg Arena, ulioko jijini Hamburg nchini Ujerumani.

Iliwahusisha nyota wenyeji wa uwanja huo, klabu ya Hamburg, waliojiita Hamburg All Stars dhidi ya marafiki wa Ronaldo na Zidane, ambao ni mabalozi wa Shirika la Maendeleoa la Umoja wa Mataifa (UNDP), iliyolenga kukusanya fedha za kupambana na umaskini katika Pembe ya Afrika, kwa gawanyo la theluthi mbili ya mapato.

Katika mechi hiyo, nyota takriban 30 kutoka mataifa mbalimbali duniani, waliungana na mabalozi hao wa heshima, kucheza mechi hiyo ya hisani kuchangisha fedha hizo na kumaliza dakika 90 kwa Marafiki wa Zidane na Ronaldo kuwalaza wenyeji kwa mabao 5-4, huku nyota wakongwe wa zamani na wa sasa wakigeuka kivutio.

Nyota kama Fabio Cannavaro, Edgar Davids, Luís Figo, Pavel Nedv?d, Didier Drogba, Jörg Albertz, Sergej Barbarez na Richard Golz, wakawa sehemu ya harakati za mabalozi hao waliotazamwa na mashabiki wapatao 24,000 katika pambano hilo la tisa la ‘Match Against Poverty, mradi uliobuniwa miaka miwili iliyopita.

“Kila mwaka sisi hukutana kwa sababu moja maalum, mwaka huu tumekutana pamoja na kucheza mechi hii kwa ajili ya Africa,” anasema Ronaldo. “Na sisi tuna furaha kutangaza ujumbe huu muhimu kwa dunia, kwamba tunataka kuendelea kuisaidia na kuunga mkono harakati za kuzisaidia jamii zinazohitaji msaada,” anaongeza Ronaldo.

“Nadhani ujumbe umeeleweka vema,” aliongeza Zidane. “Daima ni jambo la kuvutia kujua kwamba watu wote mliopo hapa, mmekuja hapa kwa sababu hiyo kubwa – hamkuja kuangalia mechi kubwa tu, lakini mnajua sababu ya ziada iliyowaleta hapa.

“Hilo ni jambo muhimu. Ujumbe wa leo kwa mara nyingine unasema kwamba kuna mlolongo mkubwa wa matatizo kila mahali duniani, na ni kweli kwamba sisi ni wanaharakati na ndio maana tuko hapa, tutafanya maamuzi ya watu na ufahamu zaidi.”

"Kushiriki hapa ni tukio kubwa mno – kuunda fedha ambayo tunaweza kuchangai kupitia aina hii ya mechi dimbani, kucheza soka, kuwa furahani, zaidi ni watu kutona tena tukicheza soka dimbani," alisema beki wa zamani wa kimataifa wa Urno Fernando Couto.

“Kwa upande wetu pia ina maana kubwa, kwa kuwa tuinaweza kuonana tena na marafiki zetu, wachezaji wenzetu na wakati huo huo kucheza mpira wa miguu, ambao ni kitu akinachotufurahisha mno sisi kama wachezaji,” anamaliza Couto.

Kwa hakika faida za ‘Match Against Poverty’ ni nyingi mno na kunha haja ya nyota wetu, wadau na klabu zetu kuwa na aina hiyo ya ubunifu katika kusaidia jamii zinazowazunguka na zile zinazohitaji msaada hata kama ziko mbali kiasi gani.

Kesho ndiyo kesho katika dimba la Taifa jijini Dar es Salaam, ambako klabu mbili za Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga na Azam za jijini, zitakuwa na aina ya mechi unayoweza kuifananisha na hizo za ‘Match Against Poverty’ – hii ikiwa na nia ya kuchangisha fedha za kukomboa kontena la vifaa vya walemavu bandarini.

Ni kontena lililo na baiskeli na magongo ya kutembelea wenye aina tofauti za ulemavu, lililokwama kutokana na kukosa fedha za kulipia ushuru. Hapa kuna kila haja ya kuzipongeza klabu husika katika kuonesha kwao kuwa wanaijali mno jamii inayowazunguka, ambao ndio wadau wakuu wa soka lao.

Pambano hilo linalosubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki wa soka, litarajiwa kufanyika kesho na tayari timu zote zimeomba mashabiki kujitokeza kwa wingi ili kuunga mkono harakati hizo chanya kwa faida ya jamii ya wasionacho ama yenye kuhitaji msaada.

Sifa katika hili pia ziwafikie waratibu wa mechi hiyo Unity in Diversity Foundation (UDF), ambao wakiwa chini ya udhamini wa Simon Group kwa kumudu kuzishawishi na kuzimainisha klabu hizo na kukukbali kuingia dimbani kuchangia ukombozi wa kontena hilo.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadick anatarajia kuwa mgeni rasmi akiungana na jopo la wabunge zaidi ya 10 wa majimbo mbalimbali nchini, kushuhudia pambano hilo wakiongozwa na Naibu Waziri Elimu na Mafunzo ya Ufundi Philip Mulugo.

Soka ni mchezo unaokadiriwa kuwa na mashabiki wengi zaidi duniani kote. Kutumika katika utatuzi na usaidizi wa matukio ya kijamii, ni uamuzi unaoweza kuzaa faida nyingi kwa wakati mmoja kama nyota wa kikosi cha Marafiki wa Zidane na Ronaldo walivyoeleza hapo.

Ni wazi kuwa nyota wa klabu hizo (Yanga na Azam), kuna faida binafsi watapata kutokana na mchango wao, lakini kuna mengi yaliyo bora yatakayopatikana kwa klabu zao, soka la Tanzania na walengwa wakuu wa pambano hilo (jamii ya walemavu).

Mashabiki wa soka, kwa namna moja ama nyingine wametakiwa kuhudhuria kwa wingi, ili kutoa michango yao inayoweza kuwa midogo – lakini ikichanganywa pamoja inakuwa mikubwa na kusaidia ukombozi huo.

Wakizungumza katika mazoezi ya klabu ya Yanga juzi jijini Dar es Salaam, mashabiki wa klabu hiyo waliupongeza uongozi wa klabu hiyo kwa kukubali kushiriki katika mechi hiyo ya aina yake – kwa faida ya jamii isiyojiweza na kutaka mashabiki wote kuunga mkono kwa kuhudhuria mechi.

“Binafsi napenda niupongeze uamuzi wa busara uliofikiwa na pande zote husika, kwa maana ya klabu shiriki, waratibu na wadhamini. Walemavu ni sehemu ya jamii inayotuzunguka na kuwajali na kuwasaidia, ni jambo lisiloepukika.

“Hivyo jitihada hizi ziungwe mkono na mashabiki wote kwa kwenda kwa wingi uwanjani kuchangia kidogo walichonacho kwa faida ya wenzetu hao, ili kuonesha mapenzi yetu kwao kama wao wanavyohitaji” alisema shabiki mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Kasea Mshama mkazi wa Kigogo, Dar es Salaam.

Kimsingi ni pambano linalopaswa kuonwa moja kwa moja uwanjani na kila shabiki wa soka aliye jijini na miji ya jirani, kwani ndio njia kuu ya kuonesha upendo kwa jamii ya walemavu, inayopigania kila uchao kuheshimiwa na kuthaminiwa kama ilivyo jamii nyinginezo.

bottom of page