top of page

Habari za Kitaifa
December 11, 2011

KONTENA ZA WALEMAVU ZILIZOKWAMA ZATOLEWA

Imeandikwa na Theopista Nsanzugwanko

​Imesomwa na watu: 100; Jumla ya maoni: 0

​

KONTENA mbili zenye vifaa vya walemavu yaliyokuwa yamekwama bandarini kwa zaidi ya
mwaka mmoja kutokana deni, zimetolewa baada ya Serikali kuomba kusamehewa deni hilo.

Asasi isiyo ya kiserikali ya Unity in Diversity Foundation (UDF) ndiyo iliyoagiza vifaa hivyo kutoka kwa wafadhili waliopo nje ya nchi.

Kontena hizo zilifikishwa nchini Oktoba mwaka jana. Deni hilo la zaidi ya Sh milioni 120, linadaiwa kuwa lilitokana na Hazina kuchelewa kutoa kibali cha msamaha wa kodi na kusababisha kuwepo na tozo ya kuhifadhiwa kwa kontena hizo.

Vifaa hivyo vinavyogawiwa kwa vituo na shule za walemavu vilitolewa baada ya Naibu Waziri
wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philipo Mulugo na wabunge kufika katika bandari kavu ya Kampuni ya Tanzania Road Haulage (1980) iliyopo Kurasini na kuomba kusamehewa tozo hilo.

Baada ya Maombi hayo, Meneja wa bandari hiyo, Ally Kirro alithibitisha kutolewa msamaha wa deni hilo .

Chama Cha Mapinduzi (CCM) kupitia kwa Mweka Hazina wake, Mwigulu Nchemba kimeahidi
kulipa Sh milioni 1.7 ambazo ni lazima kulipia kontena hizo.

Mulugo alifuatana na Nchemba ambaye pia ni Mbunge wa Iramba Magharibi, Mbunge wa Viti Maalumu, Victoria Kamata na Kaimu Mkurugenzi wa Elimu Maalumu toka Wizara ya Elimu, Amani Katembo.

Akizungumza mara baada ya kupata msamaha huo, Mulugo alisema imefika wakati kuangalia
upya mfumo wa Serikali katika kutoza ushuru kwa kurahisisha utoaji wa msamaha wa ushuru kwa vifaa hivyo.

Mwigulu alisema chama kinatambua umuhimu wa vifaa hivyo kwa watu wenye ulemavu kwa ajili ya kuendesha maisha yao.

Mratibu Taifa wa UDF, Enock Bagaye aliishukuru Serikali na wabunge hao kwa kuwezesha kontena hizo kutolewa.

bottom of page